29 Desemba 2025 - 19:06
Araqchi: Umoja wa ardhi na mamlaka ya Yemen lazima vilindwe

Katika mazingira ya kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa na kijeshi nchini Yemen, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi, amesisitiza ulazima wa kulindwa umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo, akionya dhidi ya madhara ya mgawanyiko na kuingilia masuala ya ndani. Kauli hiyo imetolewa kupitia mazungumzo ya simu na mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, huku pia akigusia hali ya usalama nchini Yemen na kulaani uchokozi unaoendelea wa Israel dhidi ya Lebanon.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi, amesisitiza ulazima wa kulindwa umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala ya Yemen, kufuatia kuongezeka kwa mvutano katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.


Araqchi ametoa msimamo huo katika mazungumzo tofauti ya simu aliyofanya jana Jumapili na mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, Faisal bin Farhan Al Saud na Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan.


Katika mazungumzo yake na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Araqchi alisisitiza kuwa ramani ya kisiasa inayolenga kusitisha mapigano na kufikia suluhisho pana kupitia mazungumzo katika miezi ijayo ni lazima itekelezwe kwa vitendo.


Machafuko ya sasa nchini Yemen yalizidi kushadidi tarehe 3 Desemba, wakati vikosi vya Baraza la Mpito la Kusini (STC), vinavyoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, viliponyakua udhibiti wa mkoa wa Hadramout baada ya mapigano makali na wanamgambo wanaoungwa mkono na Saudi Arabia.


Baada ya hatua hiyo ya STC, Saudi Arabia ilifanya mashambulizi ya anga Ijumaa iliyopita, ikilenga maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vya STC.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha